×
Njia zinazo saidia kuthibiti katika Dini ya Mwenyezi Mungu

Njia zinazo saidia kuthibiti katika Dini ya Mwenyezi Mungu

Utangulizi

Hakika kila sifa kamilifu ni zinamstahiki Mwenyezi Mungu, tunamsifu na tunamuimba msaada na tunamuomba msamaha.

Na tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na shari za nafsi zetu na matendo yetu mabaya,

Mwenye kuongozwa na Mwenyezi Mungu hakuna wa kumpoteza, na mwenye kupotezwa na Mwenyezi Mungu hakuna wa kumuongoza,

na nina shahidilia kuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika, na nina shahidilia kuwa Muhamad ni mja wake na nimtume wake.

Baada ya hayo

Hakika kuthibiti kaika Dini ya Mwenyezi Mungu ni jambo lamsingi kwa kila muislam mkweli anaetaka kupita katika njia ilio nyooka kwa azima na uongofu.

Umuhimu wa jambo hilo unadhihiri katika mambo yafuatayo:

Hli ya jamii mbalimbali kwa sasa ambazo wanaishi Waislamu ndani yake, na aina za fitna na udanganyifu pamoja na vishawishi, na aina mbali mbali za matamanio ambazo kwasababu yake Dini imekuwa ngeni,

wakapata wenye kushikamana na dini mfano wa ajabu- mwenye kushikamana na Dini yake nikama mwenye kushika kaa la moto-

na hakuna shaka kwa kila mwenye akili kwamba mahitaji ya Waislamu wa zama hizi ya kujuwa njia zinazo saidia kuthibiti katika Dini ni haja kubwa kuliko haja waliyokuwa nayo enzi za watu wema walio tangulia, na inahitajika juhudi ya ziada ili kunufaika na njia hizo, kutokana na kuharibika zama hizi, na uchache wa ndugu wa kweli , udhaifu wa wasaidizi na uchache wa mwenye kujitolea kwa ajili ya kuwanusuru ndugu zake katika Dini.

Yamekithiri matukio ya watu kuritadi na kuyarudia matendo machafu waliokuwa wakiyafanya, mpaka kwa baadhi ya wanao utumikia Uislamu, jambo ambalo limepelekea Muislamu kuogopa kuwa mfano wa hao wanao geuka, kwahiyo inabdi kuzishika hizi njia zitakazo mfanya athibiti kwenye dini ili apate amani.

Mada hii ina mafungamano na moyo, ambao Mtume Rehma na amani ziwe juu yake - kuhusu moyo:

Hakika moyo wa mwanadamu unageuka geuka kuliko chungu chenye maji ambayo yanayo chemka

Imepokelewa na Ahmad vol 4Uk 6 na Haakim vol2 Uk 289 na hadithi hii ipo katika Silsilatu swahihah No.1772

Na Mtume rehma na amani ziwe juu yake anapiga mfano mwingine wa moyo kwa kusema:

Hakika umeitwa moyo kwa sababu ya kubadilika, hakika mfano wa moyo ni kama mfano wa manyoa yalioko kwenye mti yanayo peperushwa na upepo

Imepokelewa na Ahmad 4/408, nayo iko katika sahihi Aljamii 2361.

Hadithi ikafuatiwa na maneno ya Mshairi:

Hakuitwa Mwanadamu ila ni kwasababu ya kusahau, wala haukuitwa moyo ila ni kwasababu ya kubadilika badilika

Kuthibitisha huku kubadilika kwa pepo za Matamanio na shubuhaati ni jambo la khatari linahitaji njia na nyenzo kubwa zinazo lingana na ukubwa wa kazi na ugumu wake.

Njia zinazo msaidia mtu kuthibiti

Na katika rehma ya Mwenyezi Mungu mtukufu kwetu ni kwamba ametubainishia katika kitabu chake na kupitia mtume wake na katika historia yake Mtume -rehma na amani ziwe juu yake- njia nyingi zinazo msaidia Mtu kuthibiti, nina kuletea baadhi ya njia hizo ewe Msomaji mtukufu:

1: Kuielekea Qur'an:

Qur'an tukufu ni njia ya kwanza, nayo ni kamba ya Mwenyezi Mungu madhubuti, na nuru iliyo wazi, mwenye kushikamana nayo atakingwa na Mwenyezi Mungu, na mwenye kuifuata Mwenyezi Mungu atamuokoa, na mwenye kulingania watu waifuate basi ataongozwa kunako njia ilio nyooka.

Mwenyezi Mungu amezungumza uwa malengo ya kuishusha Qur'an kidogo kidogo ni kwasababu ya kuithibitisha katika nyoyo za watu,

Akasema Mwenyezi Mungu mtukufu katika kujibu upotoshaji wa makafiri

Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur'ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.

Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora.

Alfurqaan /32-33.

Kwanini Qur'an ndio chimbuko la kuthibiti katika Dini ya Mwenyezi Mungu?

Kwa sababu inapandikiza imani na inatakasa nafsi kwa kumuunganisha na Mwenyezi Mungu

Kwasababu aya za Qur'an zina shuka kwa ubaridi na amani katika moyo wa Muumini, haupatwi na upepo wa fitna, na moyo wake unatulia kwa kumtaja Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu inamzidishia Muislamu mtizamo na maadili sahihi ambayo anaweza mwanadamu kupitia mambo hayo kupambana na hali zinazo mzunguka,

Na vilevile vipimo vinavyo muandalia kuyatoa hukumu mambo basi hukumu yake haitetereki, wala maneno yake hayapingani kwa kutofautiana matukio na watu.

Kwasababu yeye anayatolea majibu mambo yenye utata yanayozuliwa na maadui wa Uislamu miongoni mwa makafiri na wanafiki, kama mifano iliyokuwepo katika zama za mwanzo za Uislamu,

Na hii ni mifano:

Ni ipi athari ya maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu?

Mola wako Mlezi hakukuacha, wala hakukasirika nawe

Al-Dhuha /3

Juu ya Mtume wa Allah rehma na amani za Allah ziwe juu yake,

Zama waliposema washirikina (Muhammad kaachwa na Mola wake...)

Tazama Swahihi Muslim iliyo shereheshwa na Nawawiy 12/156.

Ni ipi athari ya maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu?

Lugha ya huyo wanaye muelekezea ni ya kigeni, na hii ni lugha ya Kiarabu iliyo bayana

Al-Nahli /103

Zama walipodai makafiri wa Kiqureshi kwamba Muhammad rehma na amani ziwe juu yake anafundishwa na kiumbe na kwamba Qur'an anaichukuwa kwa fundi seremala Mroma aliyekuwa katika Mji wa Mkkah?

Ni ipi athari ya maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu?

Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina

Tawbah /49

Katika nafsi za Waumini pindi waliposema wanafiki:

Niruhusu wala usinifitinishe?

Je! Huku siyo kuthibitisha juu ya kuthibitisha, na kuunganisha nyoyo za Waumini, na ni kuyajibu mambo yenye utata, na kuwanyamanzisha watu wa batili?

Ni kweli naapa kwa Mola wangu.

Na jambo la kushangaza ni kwamba Mwenyezi Mungu anawaahidi Waumini katika kurejea kwao kutoka katika makubaliano ya Huadeibiyah (Sulhul Hudeybiyah) kuwa watapata ngawira nyingi watakazo zichukua katika vita ya Khaybari

Na kwamba atazifanya ngawira hizo ziwe za kwao na wao watazifuata huko

Na kwamba wanafki wataomba waende pamoja

Na Waislamu watawaambia hamtatufuata

Na wao watalazimisha waende wakitaka kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu

Na wao watesema kuwaambia Waumini bali mnatuhusudu na Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema:

Baili walikuwa hawajui isipokuwa kidogo

Kisha yanatokea hayo yote mbele ya Waumini hatua kwa hatua na ngazi kwa ngazi na neno kwa neno.

Kuanzia hapo tunaweza tuakafahamu tofauti kati ya wale ambao waliyafunga maisha yao na Qur'an na wakaielekea Qur'an kwa kuisoma, na kuihifadhi, na kuitafsiri, na kuizingatia, wanakwenda kwa maelekezo ya Qur'an, na marejeo yao ni katika Qur'an, na baina ya wale waliofanya maneno ndiyo kipaumbele kikubwa na ndio kazi yao yenye kuwashughulisha

Na laiti wale wenye kutafuta elimu wangeifanya Qur'an na tafsiri yake ndiyo kipaumbele kikubwa katika utafutaji wao.

2-

Ni kujilazimisha kufuata sheria ya Mwenyezi Mungu na kufanya matendo mema

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo

Ibrahim /27

Amesema Qataadah:

Ama maisha ya duniani Mwenyezi Mungu anawathibitisha kwa kufanya kheri na matendo mema, na Akhera Mwenyezi Mungu anawathibitisha kaburini.

Na hivohivo imepokelewa na wengi katika wema waliotangulia

Tafsiirul Qur'anil Adhwiim Liibni Kthiir, 3/421.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

lau kuwa tumewaamrisha: Jiueni, au tokeni majumbani kwenu, wasingeli fanya hayo ila wachache tu miongoni mwao. Na lau kama wangeli fanya walio waidhiwa ingeli kuwa bora kwao na uthibitisho wa nguvu zaidi

Nisaa /66

Yaani juu ya haki.

Na hili liko wazi, na kama si hivyo je! Tunategemea kuthibitishwa watu wavivu wasiofanya matendo mema watakapoona fitna vichwani mwao na wakaelekezwa na maneno ya watu?!

Lakini wale walio amini na wakatenda matendo mema Mola wao anawaongoza kwa imani zao kunako njia iliyo nyooka.

Kwasababu hiyo Mutume rehma na amani ziwe juu yake- alikuwa anadumu katika kufanya matendo mema, na ibada iliyopendeza kwake ni ile aliyodumu nayo hata kama ilikuwa ni ndogo.

Na Maswahaba zake walikuwa wanapofanya ibada wanaithibitisha. Na Mama Aisha radhi za Allah ziwe juu yake anapofanya ibada analazimiana nayo.

Na Mtume rehma na amani za Allah ziwe juu yake alikuwa anasema:

Mweyne kudumu na rakaa kumi na mbili ataingia Peponi

Sunani Tirmidhy 2/273, na amesema: Hadithi ni nzuri na ni sahihi.

Na ipo katika Swahihi Nasaai 1/388, na Swahihi Tirmidhy 1/131.

Yaani Sunnah za Kabliyyah na Baadiyyah.

Na katika Hadithil Qudsiy:

Na mja wangu haachi kujikurubisha kwangu kwa kuswali Swala za Sunnah isipokuwa nitampenda

Imepokelewa na Bukhar, tazama Fathul Baary 11/340.

3-

Ni kuzingatia visa vya Manabii na kuvisoma kwa ajili ya kuvifuata na kuvifanyia kazi

Na ushahidi juu ya hayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini

Huud /120.

Hazikuteremka Aya hizo katika zama za Mtume rehma na amani ziwe juu yake ili ziwe vipumbazo au vichekesho,

Bali zimeshuka kwa malengo makubwa nayo ni kuuthibitisha moyo wa Mtume rehma na amani ziwe juu yake na nyoyo za Waumini pamoja nae.

Lau ukizingatia ewe ndugu yangu maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!

Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!

Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri.

Al-Ambiyaa /68-70

Na amesema Ibni Abas:

Yalikuwa maneno ya mwisho ya Ibrahim alipotupwa katika moto: Ananitosha Mwenyezi Mungu na Yeye ndiye mbora wa kutegemewa

Fat'hul Baary 8/22

Ukitafakari kisa hiki Je! Huhisi maana yoyote miongoni mwa maana za kuthibiti katika Dini ikiingia katika nafsi yako mbele ya uovu na adhabu?

Lau ukizingatia kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kisa cha Mussa:

Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Mussa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!

(Mussa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!

Al-Sshuaraa /61-62.

Unapo zingatia kisa hiki Je! Huhisi maana nyingine katika maana za kuthibiti pindi unapokutana na wenye shida, na kuthibiti wakati wa shida katikati ya ukelele wa wale waliokata tamaa?

Lau utaangalia matukio ya kisa cha wachawi wa Firauni, utaona mfano wa ajabu wa watu waliothibiti katika haki baada ya kubainikiwa.

Je! Huoni kwamba maana kubwa katika maana za kuthibiti maana hiyo ikitulizana katika nafsi ya vitisho vya mtu dhalimu na huku akisema:

(Firauni) akasema: Oh! Mnamuamini kabla sijakupeni ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliye kufundisheni uchawi. Basi kwa yakini nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakutundikeni misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi aliye mkali wa kuadhibu na kuiendeleza adhabu yake.

Twaha /71.

Kuthibiti kwa Waumini wachache waliothibiti bila ya kurudi nyuma na huku wakisema:

Wakasema: Hatutokukhiari wewe kuliko ishara waziwazi zilizo tujia, na kuliko yule aliye tuumba. Basi hukumu utavyo hukumu; kwani wewe unahukumu haya ya maisha ya duniani tu.

Twaha /72.

Vilevile kisa cha Muumini kilichopo katika Surat Yasin, na Muumini katika watu wa Firauni na watu wa mapangoni na wengineo, kuthibiti katika Dini kumekaribia kuwa ndio somo kubwa kuliko yote.

4-

Ni Dua

Miongoni mwa sifa za waja wa Mwenyezi Mungu Waumini ni kwamba wao wanamuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumuomba awathibitishe:

(Na hao husema): Mola wetu Mlezi! Usizipotoze nyoyo zetu baada ya kwisha tuongoa

Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utusaidie tuwashinde watu Makafiri

Na pindi zilipokuwa

nyoyo za wanadamu zote zipo baina ya vidole viwili katika Vidole vya Mwenyezi Mungu kama moyo wa mtu mmoja anaufanya atakavyo.

Ameipokea Imamu Ahmad na Muslim kutoka kwa Ibni Omar kutoka kwa Mtume rehma na amani ziwe juu yake.

Tazama Swahihi Muslim iliyo shereheshwa na Nawawiy 16/204.

Mtume wa Allah -rehma na amani ziwe juu yake alikuwa akikithirisha kusema:

Ewe mwenye kuzigeuza nyoyo uthibitishe moyo wangu katika Dini yako.

Ameipokea Tirmidhiy kutoka kwa Anasi kutoka kwa Mtume rehma na amani ziwe juu yake, Tuhfatul Ah'wadhiy 6/349, nayo ni katika Swahihil Jaamii 7864.

5-

Ni kumtaja Mwenyezi Mungu

Nayo ni katika sababu kubwa za kuthibiti.

Zingatia katika makutano haya kati ya mambo mawili katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.

Al Anfaal /45.

Akajaalia ni katika sababu kubwa zinazo msaidia mtu kuthibiti katika Jihadi.

Na zingatia miili ya watu wa Fursi na Roma ni jinsi gani iliwafanyia khiyana ilihali wanaihitajia

maneno yaliyopo katika mabano yamechukuliwa katika maneno ya Ibnil Qayyim Allah amrehem katika kitabu chake Al-Daau wa Al-Dawaa.

Pamoja na idadi ndogo lakini maandalizi ya wenye kumtaja Mwenyezi Mungu ni mengi.

Ni kitu gani kilicho msaidia Nabii Yusuf kuthibiti katika fitna ya mwanamke mzuri na mwenye cheo pindi alipo mtamani kimapenzi?

Je! Hakuingia katika ngome ya Mwenyezi Mungu pindi aliposema "najikinga kwa Mwenyezi Mungu" kwa neno yakavunjika mawimbi ya matamanio kwenye uzio wa ngome yake?

Na hivo ndivyo inavyokuwa kazi ya adhkari katika kuwathibitisha Waumini.

6-

Ni Muislamu kuwa na pupa ya kupita katika njia sahihi

Na njia pekee iliyo sahihi ambayo ni wajibu kwa kila Muislamu kuipita ni njia ya Ahlu Sunnah waljamaa njia ya kundi lililo nusuriwa na kundi lililo okoka, watu wa itikadi iliyo safi na njia iliyo salimika na kufuata mwenendo wa Mtume na dalili, na kuwapambanua maadui wa Mwenyezi Mungu na kuwatenga watu wa batili.

Na ukitaka kujua thamani ya hayo katika kuthibiti kunako Dini ya Allah zingatia njia za nafsi yako: Kwanini waliotangulia na wa zama hizi wengi walipotea na wakawa katika mshangao na hawakuthibiti katika njia iliyo nyooka wala hawakufa katika njia hiyo?

Au waliifikia baada ya kumalizika sehemu kubwa katika umri wao na wakapoteza muda wao wenye thamani katika maisha yao?

Utawaona miongoni mwao wanahama kutoka katika vituo vya uzushi na upotevu na kwenda katika falsafa na elimu ya maneno na wengine wanatoka katika kundi la Muutazila na kwenda katika makundi yenye kupotosha dalili na kuzigeuza pamoja na kuzitumia katika maana zisizokuwa sahihi, na wengine wanatoka katika njia za Kisufi na kwenda kwenye makundi mengine ya upotovu.

Na hivyohiyvo watu wa bid'aa wanapatwa na mshangao na kubabaika, angalia ni jinsi gani watu wa elimu ya maneno walivyo nyimwa kuthibiti katika Dini wakati wa kufa kwao, watu wema waliotangulia wanasema:

Watu wengi wenye mashaka wakati wa kufa ni watu wa maneno

Lakini fikiria na uzingatie je! Kuna yeyote katika Ahlu Sunnah wal Jamaa aliyeacha njia yake kwasababu ya kuichukia baada ya kuijua na akaisoma na akashika njia hiyo?

Anaweza akaiacha kwasababu ya matamanio na shubha kutokana na udhaifu wa akili yake, lakini haiachi kwasababu ameona iliyokuwa sahihi kuliko hiyo au imembainikia kuwa ni batili.

Na kinacho yasadikisha hayo ni maswali ya Hiraqli kwa Abuu Sufiyan kuhusu wafuasi wa Muhammad rehma na amani ziwe juu yake,

Hiraqli alimuuliza Abuu Sufiyan:

Je! Anaritadi yeyote kutoka katika Dini yake baada ya kuingia?

Abuu Sufiyan akasema: Hapana.

Kisha Hiraqli akasema:

Na hivyohivyo ndivyo inavyokuwa imani pindi inapochanganyika na bashasha ya moyo

Ameipokea Bukhary, Fat'hul Baary 1/32

Tulisikia sana kuhusu watu wakubwa waliohimia katika nyumba za watu wa bid'aa na wengine Mwenyezi Mungu aliwaongoza wakaacha batili wakahamia katika madhehebu ya Ahlu Sunnah wal Jamaa wakiwa ni wenye kuyachukia madhehebu yao ya zamani, lakini je! Tumewahi kusikia kinyume chake?!

Ukitaka kuthibiti katika Dini ya Allah ni lazima ufuate njia ya Waumini.

7-

Ni malezi

Malezi ya kiimani na ya kielimu yanayo kuwa hatua baada ya hatua, ni sababu ya msingi miongoni mwa sababu zinazo mfanya mtu athibiti katika Dini.

Malezi ya kiimani: Ni yale yanayo huisha moyo na dhamira kwa mtu kuwa na khofu na matarajio na mapenzi, imani inayopingana na ugumu wa moyo unaosababishwa na mtu kuwa mbali na Qur'an na Sunnah, na kufuata maneno ya watu.

Malezi ya kielimu: Ni malezi yanayo tegemea dalili sahihi yanayopingana na kuiga na vyanzo vibaya.

Malezi ya kimaarifa: Ni malezi ambayo hayajui njia za waovu na yanasoma mipango yote ya maadui wa Kiislamu na hali za kimazingira na yanayo tokea ndani yake, malezi yanayo pingana na matakwa ya nafsi na mtu kudondokea katika mazingira yaliyo pangwa na watu.

Malezi ya hatua kwa hatua: Ni malezi ambayo yanampeleka Muislamu hatua kwa hatua, yanampandisha katika ngazi za ukamilifu kwa mipangilio iliyo pimwa, malezi yanayo pingana na kufanya mambo kwa kuruka ruka bila ya mpangilio.

Na ili tudiriki umuhimu wa hivi vipengele miongoni mwa vipengele vya kuthibiti katika Dini inabidi turudi katika historia ya Mtume rehma na amani ziwe juu yake na tuziulize nafsi zetu.

Ni vipi vyanzo vya kuthibiti Maswahaba wa Mtume rehma na amani ziwe juu yake wakiwa katika Mji wa Makkah, katika zama za mateso?

Vipi alithibiti Bilali na Khabaab na Musw'ab na watu wa Yasir na wengine katika wale walio dhoofishwa mpaka Maswahaba wakubwa waliofanyiwa vikwazo katika Shuab ya Banii Hashim na mengineyo?

Je! Inawezekana kuthibiti kwao kulikuwa bila ya malezi kutoka kwa Mtume malezi ambayo yaliwafanya wawe mashujaa?

Tumchukue Swahaba mmoja mfano wa Khabaab radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake ambae bwana wake alikuwa anachemsha chuma mpaka kinakuwa chekundu kisha anamchoma mgongoni akiwa hana nguo mpaka kinapoa, ni kitu gani kilicho mfanya avumilie mateso yote hayo?

Na Bilali alipowekewa jiwe juu ya mwili wake akiwa amelazwa chini wakati wa joto kali, na akiwa amefungwa minyororo kila mahali.

Na swali lingine linachimbuka katika zama ambazo Mtume alikuwa Madina, ni nani aliye thibiti pamoja na Mtume rehma na amani ziwe juu yake katika vita vya Hunayni pindi Waislamu walipo shindwa?

Je! Walikuwa ni wageni katika Uislamu na Waislamu waliokuwepo katika Fat'hu Makkah ambao hawakukaa muda mrefu katika Madrsa ya Mtume na wale wengi wao walitoka kwasababu ya ngawira?

Si hivyo! Hakika wengi waliothibiti ni wale waliokuwa Waumini safi waliopata kiwango kikubwa cha malezi ya Mtume rehma na amani ziwe juu yake.

Lau kusingekuwa na malezi bora je! Hao wangethibiti katika Dini ya Allah?

8-

Ni kuwa na uhakika na njia unayoifuata

Hakuna shaka ya kwamba kila unapozidi uhakika wa njia anayopiata Muislamu, kuthibiti kwake katika njia hiyo kunakuwa ni kukubwa, na kudumu katika hilo kuna njia nyingi miongoni mwazo ni:

Ni kuhisi kwamba njia iliyonyooka unayopita - ewe ndugu yangu - siyo mpya wala haija anzishwa katika karne yako wala katika zama zako,

bali ni njia nzuri ambayo wameipitia waliokuwa kabla yako katika Mitume na wasema kweli na Wana chuoni na Mashahidi na watu wema, basi ugeni wako unaondoka na upweke unabadilika kuwa faraja, na huzuni kuwa furaha, kwasababu unahisi kwamba wote hao ni ndugu zako katika njia na mfumo.

Ni kuhisi kuwa umechaguliwa,

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Alhamduli LLah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu! Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa.

Al-Namli /59.

Na alisema:

Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateuwa miongoni mwa waja wetu.

Fatwir /32.

Na alisema:

Na kadhaalika Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakufundisha tafsiri ya mambo.

Yusuf /6.

Kama Mwenyezi Mungu alivyo wachagua Mitume basi watu wema wana fungu katika huo uteuzi na fungu hilo ni elimu waliyo irithi kutoka kwa Mitume.

Unahisi vipi lau Mwenyezi Mungu angekuumba jiwe, au mnyama, au kafiri, au mwenye kulingania mambo ya uzushi, au mtu muovu, au Muislamu asiye lingania kunako Uislamu, anaye lingania katika tofauti zenye makosa?

Huoni kwamba kuhisi kwako kuwa umechaguliwa na Mwenyezi Mungu na amekujalia kuwa mlinganiaji wa Ahlu Sunnah wal Jamaa ni katika sababu za kuthibiti kwako katika Mfumo na njia yako?

9-

Ni kushiriki katika kulingania nkatika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu

Nafsi kama haikushughulishwa inaharibika, na ikiharibika inaoza,

na katika nyanja za kuishughulisha nafsi ni kulingania katika njia ya Mwenyezi Mungu, na hiyo ni kazi ya Mitume, na inaiokoa nafsi kutokana na adhabu, na ndani yake nguvu zinaongezeka, na mafanikio yanaonekana

kwasababu hiyo lingania, na usimame imara kama ulivyo amrishwa

Na haifai kusema kwamba fulani haendelei wala harudi nyuma kwasababu nafsi kama hukuishughulisha katika ibada basi itakushughulisha katika maasi,

Na Imani inazidi na kupungua.

Na kulingania katika Manhji sahihi - kwa kutumia muda, fikra, mwili na Kutumia ulimi kuongea, kiasi kwamba ulinganizi ndiyo inakuwa kipaumbele chake cha kwanza na ndiyo shughuli yake inayo mshughulisha - anakata njia ya Shetani ya kujaribu kupotosha pamoja na fitna.

Ongeza juu ya hayo kwa yele yanayo tokea katika nafsi ya Mlinganizi miongoni mwa kuhisi changamoto katika kupambana na vipingamizi, na wapinzani, na watu wa batili, naye akiwa anapita katika harakati zake za Kidaawah, basi imani yake inazidi, na misingi yake inakuwa imara.

Ukiongeza malipo makubwa yanayo patikana katika Daawah, kwa hakika Daawah hiyo ni njia miongoni mwa njia zinazo mfanya mtu athibiti katika Dini, na ni kinga inayo mfanya mtu asirudi nyuma,

Kwasababu yule anaeshambulia hahitaji kinga,

Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na Walingamizi anawathibitisha na kuwapa nguvu, na Mlinganiaji ni kama daktari anapiga vita maradhi kwa uzoefu wake na elimu yake, na kwa kuyapiga kwake vita maradhi ili yasiwapate wengine basi yeye huwa mbali na maradhi zaidi ili yasimpate.

10-

Ni kuwategemea walio madhubuti

Watu hao ni wale wenye sifa alizotueleza Mtume rehma na amani ziwe juu yake:

Hakika miongoni mwa watu kuna watu ambao ni funguo za kheri na ni kufuli za shari.

Hadithi hii ni nzuri ameipokea Ibni Maajah kutoka kwa Anasi kutoka kwa Mtume 237, na kutoka kwa Ibni Abii A'swim katika Kitabu cha Sunnah 1/127, na tazama Kitabu Silsilatu Swahiiha 1332.

Ni kuwatafuta Wanachuoni na watu wema na Walinganiaji na Waumini, na kujikurubisha kwao ni usaidizi mkubwa katika kuthibiti.

Na imetokea katika historia ya Kiislamu fitna ambazo Mwenyezi Mungu aliwathibisha Waislamu kwasababu ya watu fulani.

Na miongoni mwa hayo ni yale aliyosema Ally bin Al Madiny Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu:

Mwenyezi Mungu aliipa nguvu Dini kwasababu ya Abubakar Swidiiq siku watu walipo ritadi, na aliipa Dini nguvu kwasababu ya Ahmadi siku watu walipopata shida.

Na zingatia yale aliyosema Ibnul Qayyim Mwenyezi Mungu amrehemu kuhusiana na juhudi za Shekh wake Sheykhul Islaamu katika kuthibiti:

Na tulikuwa pindi inapo tuzidia khofu na tukawa na dhana mbaya, na tukapata dhiki katika ardhi tunamwendea, na tunamuona na tunasikiliza maneno yake basi mazito yote yanatuondokea, na nyoyo zinakunjuka na kupata nguvu na yakini pamoja na utulivu, utakasifu ni Mwenyezi ambaye aliwaonyesha waja wake Pepo yake kabla hawajakutana naye na akawafungulia milango yake wakiwa duniani, na akawapa upepo wa Peponi na marashi yake jambo lilifanya wamalize nguvu zao katika kuitafuta na kushindana kwasababu ya Pepo.

Al-Waabil Al-Swaib Uk. 97.

Kwasababu hiyo unaonekana wazi udugu wa Kiislamu ni kama chimbuko la msingi la kuthibiti, basi ndugu zako wema na viigizo vyema na wlezi hao ndio msaada wako katika njia yako, na ndiyo nguzo madhubuti unayo iegemea, wanakuthibitisha kutokana na waliyokuwa nayo miongoni mwa Aya za Menyezi Mungu na Hekma.

Lazimiana nao na uishi pembezoni mwao, na tahadhari na upweke wasije wakakuchukua Mashetani kwasababu Mbwa mwitu anamla kondoo aliyejitenga.

11-

Ni kuwa na uhakika na nusra ya Allah na kwamba Uislamu utapata mustakbali mzuri

Tunahitaji kuthibiti wakati nusra inapochelewa, ili miguu isiteleze baada ya kuthibiti,

Alisema Allah Mtukufu:

Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanao subiri

ala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri

Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.

Al Imran /146-148.

Na pindi Mtume rehma na amani ziwe juu yake alipotaka kuwathibitisha Maswahaba wake wanaoadhibiwa aliwaeleza kwamba Uislamu utakuwa mustakbali mzuri katika nyakati za kuadhibiwa na nyakati za shida ni kitu gani aliwambia?

Imekuja katika hadithi ya Khabaab iliyo katika Sahihi Bukhary kutoka kwa Mtume rehma na amani ziwe juu yake:

Na Mwenyezi Mungu atatimiza jambo la Dini hii mpaka msafiri atatembea kutoka Swanaa mpaka Hadhara Mauti bila ya kuogopa chochote isipokuwa Mwenyezi Mungu, ila atawaogopea kondoo wake kutokana na mbwa mwitu.

Imepokelewa na Bukhar, tazama Fathul Baary 7/165.

Akabainisha hadithi inayo onyesha bishara njema ya kwamba mustakbali wa Uislamu utakuwa mzuri, na ubainifu huo kwa watu ambao ni wageni katika Uislamu ni jambo la muhimu katika kuwalea juu ya kuthibiti.

12-

Ni kujua uhakika kuhusu batili na kuto kudanganyika nayo

Katika kauli ya Allah Mtukufu:

Kabisa kusikudanganye kubakia kutangatanga kwa walio kufuru katika nchi.

Al-Imran /196

Kuwaliwaza Waumini na kuwathibitisha.

Na katika kauli yake Allah Mtukufu:

Basi lile povu linapita kama takataka tu basi.

Al-Raad /17.

Ni mazingatio kwa wenye akili katika kutoiogopa batili na kutojisalimisha katika batili.

Na katika njia za Qur'an ni kuwafedhehesha watu wa batili na kuyaweka wazi malengo yao na njia zao,

Na ndio hivi tunavyo zieleza Ishara ili ibainike njia ya wakosefu.

Al-An'aam /55.

Ili Waislamu wasiichukue Dini kwa njia ya ghafla (haraka) na ili wajue Uislamu ni wapi unatoka.

Na ni mara ngapi tumesikia na tumeona harakati zilizo anguka na Walinganiaji walio teleza wakashindwa kuthibiti pindi walipo pewa mtihani bila ya kutarajia kwasababu ya kutokuwajua maadui zao.

13-

Ni kukusanya tabia njema zinazo saidia kuthibiti

Na ya kwanza katika hizo ni Subra, hadithi iliyokuja katika Swahihi mbili:

Na hakupewa mtu yeyote kitu kilicho bora na kipana zaidi kuliko Subra.

Ameipokea Imamu Bukhary katika Kitabu cha Zakka mlango unaoelezea juu ya kujizuia kuomba, na imepokelewa na Imamu Muslimu katika Kitabu cha Zakka mlango wa ubora wa kujizuia na kuwa na Subra.

Na Subra iliyo ngumu ni wakati wa kutokea msiba, mtu anapopatwa na jambo alisilotegemea anapata udhaifu na anaondokewa na uthibiti pindi anapokosa Subra.

Zingatia katika yale aliyosema Ibni Jauziy Allah amrehemu:

Nilimuona mtu mzima aliyekaribia miaka thamanini na alikuwa anadumu na swala ya jamaa akafa mjukuu wake, akasema: Haipaswi kwa yeyote kuomba, kwasababu Mwenyezi Mungu hajibu. Kisha akasema: Hakika Mwenyezi Mungu anafanya inadi kwasbabu hatuachii hata mtoto.

Rejea Kitabu, Al-Thabaat Indal Mamaat Liibni Al-Jauziy, Uk. 34

Ametukuka Mwenyezi Mungu kutokana na hayo aliyosema kutukuka kuliko kukubwa.

Zama Waislamu walipopatwa na msiba katika vita vya Uhdi hawakutarajia kupatwa na msiba ule, kwasababu Allah aliwapa ahadi ya kuwanusuru, Mwenyezi Mungu akawafundisha somo kubwa kwa kutumia damu na mashahidi wengi waliokufa:

Nyinyi - ulipo kusibuni msiba ambao nyinyi mmekwisha watia mara mbili mfano wa huo - mnasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo umetoka kwenu wenyewe.

Al-Imran /165

Nini kilicho tokea katika nafsi zao?

mpaka mlipo shindwa na mkazozana juu ya amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyo yapenda. Wapo miongoni mwenu wanao taka dunia.

14-

Ni wasia wa mtu mwema

Muislamu anapopatwa na fitna (Mtihani) na akajaribiwa na Mola wake ili amuweke mbali na mtihani huo, inakuwa miongoni mwa sababu za kuthibiti kwake ni Mwenyezi Mungu kumuandalia mtu mwema atakaempa mawaidha na kumthibitisha, basi yanakuwa ni maneno ambayo Mwenyezi Mungu anamnufaisha nayo na kumpa nguvu,

Na maneno hayo yanakuwa yamekusanya ndani yake ukumbusho wa Mwenyezi Mungu na siku ya kukutana nae na Pepo yake na Moto wake.

Ewe ndugu yangu, hii ni mifano mingine katika historia ya Imamu Ahmad Allah amrehemu, ambae aliingia katika dhiki na shida kisha akatoka akiwa kama dhahabu iliyo safishwa.

Alipelekwa kwa kiongozi Maamuni akiwa amefungwa minyororo, na akaahidi kumpa adhabu kali kabla hajafika kwake, mpaka mtumishi wa Imamu Ahmad akasema:

Inaniwea ngumu ewe Baba Abdallah, hakika Maamuni ameutoa upanga wake katika ala yake hajawahi kufanya hivyo, na anaapa kwa ndugu zake wa karibu wanaotokana na ukoo wa Mtume rehma na amani ziwe juu yake, ikiwa hukumjibu kauli ya kuumbwa kwa Qur'an atakuuwa kwa kutumia panga lile

Rejea Kitabu Al-Bidaayatu wa Al-Nihaayah 1/332.

Na hapa watu wenye akili na wenye busara wanaitumia fursa ya kukutana na Imamu wao ili wampe maneno ya kumthibitisha;

Katika Kitabu Al-Siyar liDhahbiy 11/238 kutoka kwa Abii Jaafar Al-Ambaary alisema:

Pindi alipobebwa Imamu Ahmad kupelekwa kwa Maamuni niliambiwa, nikavuka mto Furaat, mara nikamuona amekaa kwa Hakimu nikamsalimia. Akasema: Ewe Abuu Jaafar bila umekuja kwasababu ya matatizo. Nikasema: Ewe Imamu, leo hii wewe ni kichwa na watu wanaokufuata, naapa kwa Allah ukijibu ya kwamba Qur'an imeumbwa basi watu wote watajibu hivo, na ikiwa hukujibu hivo watu wengi watakataa kusema kuwa Qur'an imeumbwa, pamoja na hayo ikiwa huyu Maamuni hakukuuwa hakika wewe utakufa tena hakuna budi lazima ufe, basi muogope Mwenyezi Mungu na wala usijibu. Imamu Ahmad akawa analia na huku akisema: Mashaa Allah. Kisha akasema: Ewe Abuu Jaafar rudia maneno yako, nikayarudia na huku akisema: Mashaa Allah.

Na akasema Imamu Ahmad akiwa katika safari yake kwenda kwa Maamuni:

Tulifika katika nyumba yake usiku wa manane, akatujia mtu akasema: Ni yupi Ahmad bin Hambali. Akaambiwa ni huyu hapa. Kwa uzuri kabisa akasema: Usiwe na wasiwasi, kisha akasema: Ewe Imamu hakuna tatizo wewe ukiuliwa hapa na ukaingia Peponi, kisha akasema: Nakuaga na Mwenyezi Mungu akuhifadhi, na akaondoka. Nikaulizia kuhusu mtu huyo, nikaambiwa ni Mwarabu katika kabila la Rabia anafanya kazi ya Sufi kijijini, jina lake anaitwa: Jaabir bin A'mir anajulikana kwa kheri.

Rejea Kitabu, Siyar A'alaami Al-Nubalaa 11/241.

Na katika Kitabu Al-Bidaayah Wa Al-Nihaayah: Bedui mmoja alimwambia Imamu Ahmad:

Ewe Imamu hakika wewe ni mgeni wa watu usiwe mkosi kwa watu, na hakika wewe ni kichwa cha watu leo tahadhari juu ya kuwajibu yale wanayo yataka, ikawa ni sababu ya watu kuyafuata kisha ukabeba madhambi yao siku ya Qiyama, na ikiwa unampenda Mwenyezi Mungu basi vumilia kutokana na hali uliyo nayo, hakika hakuna baina yako wewe na Pepo isipokuwa ni kuuliwa.

Amesema Imamu Ahmad:

Na maneno yake yaliitia nguvu azma yangu kutokana na hali niliyokuwa nayo ya kukataa yale wanayo nilazimisha niyakubali.

Rejea Kitabu Al-Bidaayah wa Al-Nihaayah 1/332.

Na katika riwaya nyingine Imamu Ahmad alisema:

Sikuwahi kusikia maneno yaliyo tokea kutokana na jambo hili yenye nguvu zaidi kuliko maneno ya yule Bedui aliyo niambia katika Mji wa Rahbat Twauq Mji uliopo baina ya Riqa na Bagdadi kando ya mto Furaat, alisema: Ewe Ahmad ikiwa haki itakuuwa basi umekufa shahidi, na ukiishi basi utaishi ukiwa ni mwenye kusifiwa. Moyo wangu ukapata nguvu.

Rejea Kitabu, Siyar A'alaami Al-Nubalaa 11/241.

Na anasema Imamu Ahmad kuhusu kijana aliye ongozana naye Muhammad bin Nuh aliyethibiti pamoja nae katika fitna:

Sikuona yeyote mwenye umri mdogo na mwenye elimu ya kawaida, akiwa ni mwenye kukabiliana na amri ya Mwenyezi Mungu kuliko Muhammad Nuh, hakika mimi nina tarajia Mwenyezi Mungu awe amekhitimisha mambo yake kwa kheri. Siku moja liniambia: Ewe Baba Abdallah, tahadhari sana hakika wewe siyo kama mimi, wewe ni mtu wa kuigwa, watu wameinua shingo zao kwako wewe wakisubiri kitakacho toka kwako, basi Muogope Mwenyezi Mungu na uthibiti juu ya amri ya Mwenyezi Mungu. Akafa nikamswalia na nikamzika.

Rejea Kitabu, Siyar A'alaami Al-Nubalaa 11/242.

Mpaka wafungwa waliokuwa wakiswalishwa na Imamu Ahmad akiwa amefungwa minyororo walisaidia kumfanya athibiti.

Alisema Imamu Ahmad akiwa katika kifungo:

Mimi sijali kutokana na kifungo kwasababu jela na nyumba yangu ni kitu kimoja, wala siogopi kuuliwa kwa upanga, ninaogopa fitna ya viboko, mmoja katika wafungwa akamsikia akasema: Usijali ewe Baba Abdallah hivyo viboko unapigwa viwili tu, kisha hutajua viboko vingine wapi vimepigwa ni kama vimeondoshwa.

Rejea Kitabu, Siyar A'alaami Al-Nubalaa 11/240.

Fanya bidii ewe ndugu mtukufu kutafuta wasia kwa watu wema na uandike pindi utakapo somewa.

Utafute kabla ya safari ukiogopea mambo ambayo yanaweza kukutokea.

Utafute wasio wakati wa mitihani na majaribu, au kabla ya kupata shida inayo tarajiwa.

Utafute wasia huo pindi utakapopata cheo au ukarithi mali na utajiri.

Na ithibitishe nafsi yako, na wathibitishe wengine na Mwenyezi Mungu ni kipenzi cha Waumini.

15-

Ni kuzingatia Neema za Peponi na adhabu za Motoni na kukumbuka umauti

Na Pepo ni Mji wa furaha, na ni sehemu nzuri isiyo na huzuni, na ndiyo mafikio ya safari ya Waumini, na nafsi imeumbwa katika mazingira ya kutojitoa muhanga na kufanya ibada na kuthibiti isipokuwa kwa malipo yatakayo ipunguzia nafsi mchoko, na malipo hayo yatamrahisishia kukidhi haja ya maisha yake kutokana na uzito na mashaka.

Mtu anaejua malipo ya kazi yake basi uzito wa kazi unapungua, na ataendelea kufanya kazi kwasababu ikiwa hakuthibiti katika kazi Pepo itampita ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, kisha hakika ya nafsi inahitaji kitu kitakacho inyanyua kutoka katika udongo wa ardhi na kuelekea katika ulimwengu wa juu.

Na Mtume rehma na amani ziwe juu yake alikuwa akitumia kuitaja Pepo katika kuwathibitisha Maswahaba zake,

Katikia hadithi nzuri na sahihi alipita Mtume rehma na amani ziwe juu yake kwa Yasir na Ammaar na Mama yake na Ammaar hali ya kuwa wanaadhibiwa kwasababu ya kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mtume rehma na amani ziwe juu yake akawaambia:

Fanyezi subra enyi familia ya Yasir hakika mafikio yenu ni Peponi

Imepokelewa na Imamu Haakim 3/383

Nayo ni hadithi nzuri na sahihi, rejea chanzo chake katika Fiqhi Al-Siirah iliyo hakikishwa na Imamu Al-Albaany Uk. 103.

Na vilevile Mtume rehma na amani za Allah ziwe juu yake alikuwa akiwaambia watu wa Madina (Answar):

Hakika nyinyi baada yangu mtakutana na hali ya ubinafsi wa watu kukusanya mali na kuwanyima wenye kustahiki, sasa subirini mpaka tutakapo kutana katika Haudhwi.

Wamekubaliana Bukhari na Muslim.

Na vilevile mwenye kuzingatia hali ya makundi mawili watu wema na waovu katika makaburi yao, na kufufuliwa kwao, na kuhesabiwa kwao, na katika mizani, na wakati wa kupita katika njia nyembamba siku ya Qiyama, na mafikio mengine ya Akhera.

Kama ilivyo kwamba kukumbuka kifo kunamkinga Muislamu kutokana na kujiuwa, na kunamsimamisha katika mipaka ya Allah hawezi kuivuka.

Kwasababu atakapojua kwamba kifo ni kitu kidogo kuliko athari ya unyayo wake, na kwamba kifo chake kinaweza kutokea baada muda mchache, vipi nafsi yake itampambia kupotea au kuendelea upotevu,

Na kwa ajili hiyo Amesema Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake:

Kithirisheni kukumbuka kitu kinacho vunja ladha ya maisha (Kifo).

Ameipokea Imamu Tirmidhiy 2/50 na akaisahihisha katika Kitabu Ir'waail Ghaliil 3/145.

Sehemu za Kuthibiti:

Nazo ni nyingi zinahitaji ufafanuzi, tunatosheka kutaja baadhi yake kwa ujumla katika sehemu hii:

Ya kwanza:

Kuthibiti wakati wa fitna

Mabadiliko yanayo upata moyo sababu yake ni fitna, moyo unapopatwa na fitna ya furaha au madhara hauwezi kuthibiti isipokuwa kwa watu wenye elimu na busara ambao imani zao zimeimarisha nyoyo zao.

Na miongoni mwa aina za fitna

Fitna ya mali:

Na miongoni mwao wapo walio muahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema: Akitupa katika fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao mema.

Alipo wapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza.

Al-Taubah /75-76

Fitna ya cheo

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka.

Al-Kahfu /28

Na kuhusu uhatari wa fitna mbili amesema Mtume rehme na amani ziwe juu yake:

Mtu mwenye kupupia mali na vyeo kuliko Dini ni muharibifu zaidi kuliko Mbwa mwitu wawili wenye njaa waioachiwa katika kundi la Kondoo.

Ameipokea Imamu Ahmad katika Musnad 3/460 nayo ipo katika Swahiihil Jaami'i 5496.

Na maana yake ni kwamba mtu kupupia mali na cheo vitu hivyo vina uovu zaidi katika Dini kuliko mbwa mwitu wawili wenye njaa waliochiwa katika kundi la kondoo.

Fitna ya mke:

Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao

Al-Taghaabun /14.

Fitna ya watoto:

Mtoto ni sehemu ya uoga na ni sehemu ya ubakhili na ni sehemu ya huzuni.

Ameipokea Abuu yaala 2/305 nayo ina hadithi nyengine zinazo itia nguvu, nayo ipo katika Swahiihil Jaami'i 7037.

Fitna ya kuteswa na uovu na dhulma: Na mfano mzuri katika fitna hiyo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na aliye tukuka:

Wameangamizwa watu wa makhandaki

Yenye moto wenye kuni nyingi,

Walipo kuwa wamekaa hapo,

Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia Waumini.

Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa,

Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu.

Al-Buruuj 4-9.

Na imepokelewa na Bukhary kutoka kwa Khabaab radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema:

Tulishitakia kwa Mtume rehma na amani ziwe juu yake naye akiwa amelalia burda (nguo) katika kivuli cha Al-Kaabah,

Mtume rehma na amani ziwe juu yake akasema:

Hakika ilikuwa kwa waliokuwa kabla yanu alikuwa anachukuliwa mtu na kuchimbiwa shimo chini ya ardhi kisha anawekwa katika shimo hilo kisha unaletwa msumeno, unawekwa katika kichwa chake anapasuliwa vipande viwili na anachanwa kwa chanuo la chuma katika nyama zake na mifupa yake, na adhabu hiyo haimzuii kuthibiti katika Dini yake.

Imepokelewa na Bukhar, tazama Fathul Baary 12/315.

Fitna ya Masihi Dajjaal:

Nayo ni fitna kubwa katika maisha ya dunia

Enyi watu hakika hakuna fitna yoyote kubwa iliyo wahi kutokea katika mgongo wa ardhi tangu Mwenyezi Mungu alivyo muumba Adam kuliko fitna ya Masihi Dajjaal. Enyi waja wa Allah, enyi watu: thibitini hakika mimi nitakuelezeni sifa yake ambayo hajawahi kuwaeleza Mtume yeyote kabla yangu.

Ameipokea Ibni Maajah 2/1359, tazama katika Swahiihil Jaami'i 7752.

Na kuhusu hatua za kuthibiti moyo na kuteleza kwake wakati wa fitna, amesema Mtume rehma na amani ziwe juu yake:

Nyoyo kupata fitna ni kama vile jamvi la vijiti, moyo wowote unapofanya fitna unawekewa nukta nyeusi, na moyo wowote unaokanusha fitna unawekewa nukta nyeupe, mpaka nyoyo hizo mbili zinageuka, moyo uliokataa fitna unakuwa mweupe mfano wa jiwe jeupe lililo safishwa, fitna haiudhuru kwa muda wa kudumu mbingu na ardhi, na moyo ulioingiwa na fitna unakuwa mweusi wenye rangi ya majivu mfano wa birika lenye duara lisiloweza kuthibiti katika ardhi hata kama ndani yake kuna kitu, moyo huo haujui wema wowote wala haukatazi jambo baya isipokuwa unafuata matamanio.

Ameipokea Imamu Ahmad 5/386, na Imamu Muslim 1/128, na ni tamko lake.

Maana ya jamvi lililo tengenezwa kwa vijiti: Yaani fitna zinauathiri moyo kama vile jamvi linavyo uathiri ubavu wa mtu aliye lilalia.

Na maana ya majivu: Yaani ni rangi nyeupe iliyo changanyika na weusi, na maana ya birika lenye duara: yaani limekaa kama lililo geuzwa na kupinduliwa. (Maneno hayo yamefananishwa na mtu asiyejua chochote katika Dini yake, mtu huyo ni sawa na birika lenye umbo la duara hata kama lina kitu nadani yake lakini haliwezi kuthibiti katika ardhi).

Ya Pili

Kuthibiti katika Jihadi

Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.

Al Anfaal /45.

Na miongoni mwa madhambi makubwa katika Dini yetu ni kukimbia vitani, Mtume rehma na amani ziwe juu yake alikuwa anabeba mchanga juu ya mgongo wake katika vita vya handaq huku akisema pamoja na Waumini:

Na ututhibitishe pindi tutakapo kutana na maadui

Ameipokea Imamu Bukhary katika Kitabu Al-Ghazawaat, katika mlango unao zungumzia vita vya handaki, rejea Fat'hul Baary 7/399.

Ya Tatu

Ni kuthibiti katika Manhaji

Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.

Al-Ahzaab /23

Vyanzo vyao ni vyenye thamani kuliko roho zao, ni kwenda mbele bila ya kurudi nyuma.

Ya Nne

Ni kuthibiti wakati wa kufa

Ama makafiri na waovu hakika wao wananyimwa kuthibiti nyakati za shida hawawezi kutamka Shahada wakati wa kufa,

na hii ni alama ya mwisho mbaya, kama alivyo ambiwa mtu mmoja wakati wa kufa kwake:

Sema Laa ilaaha ila LLah, akawa anatikisa kichwa chake upande wa kulia na kushoto anakataa kusema.

Na mwingine wakati wa kufa kwake akawa anasema:

Hiki ni kipande kizuri, hiki bei yake ni rahisi,

na wa tatu akawa anataja majina ya drafti.

Na wa nne akawa anaimba nyimbo, au akawa anamtaja mpenzi wake.

Kwasababu mfano wa mambo hayo ndiyo yaliyo washughulisha na kutomtaja Mwenyezi Mungu.

Na unaweza ukaonekana kwa watu hao uso mweusi au harufu mbaya, au kuto kuelekea Kibla wakati zikitoka roho zao, hakuna ujanja wa kuepukana na maasi wala nguvu za kufanya ibada isikuwa kwa kuwezeshwa na Mwenyezi Mungu.

Ama watu wema na walio shikamana na Sunnah, Mwenyezi Mungu anawathibitisha wakati wa kufa kwao, na wanatamka Shahada mbili.

Na inaweza ikaonekana kwa hao uso wenye furaha na harufu nzuri na aina ya bishara njema wakati wa kutokwa na roho zao.

Na huu ni mfano wa mmoja miongoni mwa walio wezeshwa na Mwenyezi Mungu kuthibiti wakati wa kifo, naye ni Abuu Zar'ah Al-Raaziy ni mmoja katika Maimamu wa Ahlu Sunnah Wal-Jamaa na hiki ndicho kisa chake:

Amesema Abuu Jaafar Muhammad bin Ally na mwandishi wa Abuu Zar'ah:

Alikuja kwetu Abuu Zar'ah katika Kijiji cha Bimashaharani ni Kijiji katika vijiji vya Rayyi akiwa katika hatua za wisho za kifo na alikuwa pamoja na Abuu Haatim na Ibni Waarih na Mundir bin Shaadhan na wengineo,

wakataja hadithi ya talaqiin

Mtamkisheni maiti wenu Laa ilaaha ila LLah

Na wakaona aibu kumtamkisha Abuu Zar'ah, wakasema njooni tuisome hadithi,

Ibni Waarih akasema:

Alitusimulia Abuu A'swim alitusimulia Abdul Hamid bin Jaafar kutoka kwa Swaleh, na akawa anasema Ibni Abiy na hakuendelea Ibni Waarih kusimulia hiyo riwaya,

Akasema Abuu Haatim:

Alitusimulia Bundaar alitusimulia Abuu A'swim, kutoka kwa Abdul Hamid bin Jaafar, kutoka kwa Swaleh, hakuendelea kusimulia, na wengine walika kimya,

Akasema Abuu Zar'ah akiwa katika maradhi yaliyo pelekea kifo chake na akafungua macho yake:

Alitusimulia Bundaar alitusimulia Abuu A'swim, kutoka kwa Abdul Hamid kutoka kwa Swaleh bin Abii Ghariib kutoka kwa Kathiir bin Murra kutoka kwa Muadhi bin Jabali alisema:

Alisema Mtume wa Allah Rehma na amani za Allah ziwe juu yake:

Mwenye kuwa mwisho wa maneno yake ni laa ilaaha ila LLah ataingia Peponi.

Na roho yake ikakatika Mwenyezi Mungu amrehem.

Siyar A'alaam Al-Nubalaa 13/76-85.

Na mfano wa hao Mwenyezi Mungu amewazungumzia kwa kusema:

Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa.

Fusswilat /30

Ewe Mola wetu tujaalie tuwe miongoni mwao,

Ewe Mola wetu hakika sisi tunakuomba utujaalie kuthibiti juu ya uongofu katika mambo yetu yote,

Na mwisho wa dua zetu tunasema Alhamduli LLahi Rabbil A'lamiin.